By Khadija Mbesa
Takriban watoto 27 wameuawa nchini Afghanistan ndani ya siku tatu wakati wa mapigano makali kati ya Taliban na vikosi vya serikali.
Shirika la Umoja wa Mataifa la watoto Unicef limesema kwamba, limeshtushwa na “kuongezeka kwa kasi kwa ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto”.
Taliban wamekuwa wakifanya maendeleo makubwa kote nchini wakati wanajeshi wa kigeni wakiondoka, wakichukua miji mikuu sita ya mkoa tangu Ijumaa huku wakikataa wito wa kimataifa wa kusitisha vita.
Zaidi ya raia 1,000 wameuawa kutokana na mzozo huo katika mwezi uliopita.
Katika taarifa ya Jumatatu, Unicef ilisema kuwa, unyama unaofanywa dhidi ya watoto unakua “juu siku zinavyopita”
Unicef ilisema kwamba,vifo 27 vilirekodiwa katika majimbo matatu – Kandahar, Khost, na Paktia huku baadhi ya watoto 136 wakijeruhiwa katika maeneo haya kwa siku tatu zilizopita.
“Kwa muda mrefu Afghanistan imekuwa moja ya maeneo mabaya duniani kuwa mtoto, lakini katika wiki za hivi karibuni na, kwa kweli, masaa 72 yaliyopita , hali imekuwa mbaya zaidi,” Samantha Mort wa Unicef Afghanistan aliambia BBC.
Watoto wameuawa na kujeruhiwa katika mabomu ya barabarani na wakati wa moto. Mama mmoja alisema kuwa, familia yake ilikuwa mojawapo ya wahasiriwa katika vita hivyi, wakati nyumba yao ilipigwa bomu huku ikimwacha mwanawe wa miaka kumi na majeraha mabaya mno. watoto wengi wamelazimika kulala nje baada ya kukimbia nyumba zao.
Unicef imetoa wito pande zote kuhakikisha kuwa, watoto wanalindwa.