By Martha Chimilila Mabadiliko ya Mazingira na nyakati yanasababisha wazazi wengi kukosa muda wa kufatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto. Kazi kubwa ya malezi inafanywa na wasaidizi wa kazi, hii inasababisha mmomonyoko mkubwa wa maadili. Gazeti dijiti la Mwananchi la tarehe 26.07.2021, limechapisha habari kuhusu: ‘chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya ukatili, unyanyasaji na mauaji kwa watoto’ inasababishwa na tatizo la wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto wao, na jukumu la malezi likiwa chini ya wasaidizi wa kazi za nyumbani. Bi Julieth Sopiato, Mkurugenzi wa Shule ya Msingi ya Little Acorns, Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, katika mahafali ya darasa la saba aliwasihi wazazi kwa kusema kuwa; “Wazazi tunapaswa kutenga muda wa kuwa na watoto, tangu wakina na umri mdogo na kuwafanya marafiki zetu. Hii itawasaidia kuwa na ujasiri wa kueleza changamoto wanazopitia wakiwa shule au nyumbani” “Tuwalee watoto katika uwazi, tusiache jukumu la malezi ya watoto kwa wasichana wa kazi, bibi au shangazi. Tusimame kama wazazi katika nafasi zetu. Uwazi ndiyo utamuwezesha mtoto kumueleza Mwalimu jambo lolote hata ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa na jamii inayomzunguka.” Bwana, Priscus Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo pia alisisitiza umuhimu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto kwa kusema kuwa: “Ushiriki hafifu wa malezi kwa wazazi umesababisha watoto kukua katika tabia na mienendo isiyofaa. Walimu wanapokea watoto kitabia na mienendo tofauti na muonekano wa wazazi. Hali hii imesababishwa na jukumu la malezi kuwa juu ya wafanyakazi wa ndani. Tatizo hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa jamii na nchi ambazo uchumi unakuwa kwa sasa” Source: https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/wazazi-wakumbushwa-wajibu-wa-kuwalea-watoto-kimaadili-3563550