Ni siku kadhaa baada ya kifo cha Rais wa zamani wa Kenya, Mzee Mwai Kibaki, na hatuna budi ila kumwambia buriani, huku tukikumbuka sifa zake katika sekta ya Elimu na Uchumi.
Si siri kwamba, Mwai Kibaki alipoingia madarakani kama rais mwaka wa 2003, alizindua mpango wa Elimu ya Msingi usio na Malipo na ambao uliosifiwa sana .
Huku ada zote katika shule za msingi zilifutwa.
Ni kweli kwamba hii haikuwa mara ya kwanza maudhui ya elimu ya bure kutokea kwani karo za shule za msingi zilifutwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1978 ila, kutokana na kupungua kwa usaidizi wa serikali, shule nyingi mno zilitoza maelfu ya ada za shule, na hii ilifuta kabisa lengo la mafunzo ya bure katika shule za msingi.
Mkakati wa serikali ya Kibaki ulitenga kila ruzuku ya shule za umma kulingana na uandikishaji wa wanafunzi, na hii iliwaruhusu kununua vitabu vya kiada na kukidhi gharama zingine za uendeshaji.
Hii iliongeza bajeti ya elimu kutoka asilimia12.4 ya bajeti ya taifa mwaka wa 2004 hadi asilimia17.4 mwaka wa 2005.
Mpango wa Elimu ya Msingi wa Bila Malipo uliwezesha mamilioni ya watoto hasa waliokuwa maskini kujiandikisha shuleni.
Inakadiriwa kuwa idadi ya walioandikishwa katika shule za msingi ilipanda kutoka milioni 6 mwaka wa 2000 hadi milioni 7.4 mwaka wa 2004.
Elimu ya Msingi isiyo na Malipo ilikuwa, na inaendelea kuwa, programu adhimu inayoshughulikia usawa katika upatikanaji wa elimu ya msingi.
Hata hivyo, utekelezaji wake ulikuwa na matokeo mabaya kwa usawa na ubora katika elimu.
Kwani hakukuwa na madarasa ya ziada yaliyojengwa wala walimu wa ziada kuajiriwa.
Hali ambayo ilisababisha msongamano wa madarasa na walimu waliokuwa na kazi nyingi kupita kiasi.
Kwa hakika, uwiano wa mwalimu na mwanafunzi uliongezeka kutoka mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40, hadi mwalimu mmoja kwa wanafunzi 60.
Rais wa Zamani Mwai Kibaki atabaki kuwa Rais aliyekomboa Watoto waliokuwa katika mazingira ya ufukara ili waweze kupata Elimu. Elimu ya Bure kwa Wote!
Buriani Mwai Kibaki.
Mwandishi-Khadija Mbesa