By Martha Chimilila
Mkimbizi ni mtu aliyeondoka nyumbani au nchini kwake anapoishi sababu ya kulazimishwa, kufukuzwa, vita, ubaguzi wa rangi, uanachama wa kikundi fulani cha Kijamii au Kisiasa au hofu ya kuteswa. Uganda ni moja ya nchi inayopokea wakimbizi wengi kutoka Mataifa Jirani kama Demokrasia ya Congo na Sudani Kusini, na takwimu zinaonyesha wengi wa wakimbizi hao ni watoto.
Asilimia kubwa ya watoto waliopokelewa katika vituo vya wakimbizi ni wale ambao wazazi wao wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe au kupotezana, hii ikisababishwa na mashambulizi katika nchi zao. Mashirika ya Kuhudumia wakimbizi nchini Uganda, yanakabiliwa na changamoto za kuwasaidia watoto kupata familia ambazo zitawalea. Takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi duniani (UNHCR), zinaonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi wanaopokelewa nchini Uganda ni watoto.
Bi. Chantal Munyandinda ni moja ya wale mama wanaojitolea kuwalea watoto wakimbizi nchini Uganda. Bi Chantal alikuwa kama watoto hawa mwaka 2009 na kwa sasa ameamua kuwasaidia watoto wanaokuja katika kambi za wakimbizi bila wazazi. Hata hivyo, kundi hili linahitaji kupatiwa ushauri nasaha na muongozo mara kwa mara katika umri wa ujana, la sivyo wanaweza kushiriki katika vitendo vya Kikatili vinavyokiuka haki za Kibinadamu.
Takwimu za UNHCR nchini Uganda zinaonyesha kuwa, zaidi ya watoto wakimbizi 42,000, wanatunzwa na familia za watu ambao si jamaa zao katika kambi na makao ya wakimbizi. Baadhi ya watoto wanaeleza kuwa wanaishi maisha ya kubaguliwa na kunyanyaswa, na familia zinazowalea na ndiyo maana wengine hutoroka.
Ofisi ya Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR nchini Uganda, ilitoa takwimu, kuwa zaidi ya watoto 220,000 wakimbizi wameacha shule kutokana na ukosefu wa fedha. UNHCR ilisema kuwa, inahitaji zaidi ya dola za Marekani milioni 120, kwa ajili ya miradi ya elimu kwa watoto wakimbizi. Lakini mwezi Mei 2021, Shirika liliweza pata asilimia 30 ya fedha iliyoomba na hii imekwamisha Uwezekano wa kutoa huduma hiyo kwa watoto wakimbizi.
Watoto wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Uganda, wapo katika hatari kubwa ya kukosa mahitaji muhimu kama afya, chakula na usalama wa afya zao.
Nini kifanyike ili kuweza kupunguza tatizo hili:
Ushirika kati ya nchi wahisani na wananchi wa Uganda katika kusaidia upatikanaji wa mahitaji muhimu. Wananchi pia wana jukumu la kusaidia katika malezi ya watoto hawa. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema:
“Utavuna Ulichopanda”
Source: https://www.bbc.com/swahili/habari-49676075
https://www.dw.com/sw/madhila-wanayopitia-watoto-wakimbizi-wanaowasili-uganda/a-54263413