By Martha Chimilila
Usonji ni tatizo la kinafsi na la kihisia linalowatokea watu wengi tangu utotoni na kuathiri uwezo wao wa kuwasiliana na watu wengine. Kifupi watu wenye Usonji hawana uwezo mzuri katika swala zima la Mawasiliano. Nchini Rwanda, wazazi wengi wanapata shida katika malezi ya kitaaluma kwa watoto wenye tatizo la Usonji, Bodi ya Elimu imeazimia kuandaa mtaala wa elimu unaoendana na uwezo wa akili wa watoto hawa.
Kwa muda mrefu Bi. Jacqueline Dushimirimana, amepata shida katika kupata shule sahihi kwa ajili ya binti yake, hali yake ya afya haikumruhusu kusoma katika shule zenye mitaala ya kawaida. Bi. Jacqueline aliona hali ya kiutofauti kwa binti yake na watoto wengi tangu akiwa na mwaka mmoja.
“Alikuwa hawezi kukaa sehemu moja. Alipofikisha miaka saba nilimuandikisha shule ya msingi, lakini hakuwezi kutulia sehemu moja, mara kwa mara alitoka darasani. Hakuwa akielewa anachofundishwa na walimu wake. Hii ilisababisha kutafuta ushauri wa Wataalamu wa afya”
“Tulipata ushauri wa kitabibu kutoka kwa Wataalamu tofauti wa afya, lakini hali haikubadilika. Baada ya uchunguzi yakinifu binti yangu aligundulika kuwa na tatizo la Usonji. Nilimpeleka katika Taasisi inayojishughulisha na watoto wenye Usonji. Wataalamu katika Taasisi hiyo walithibitisha kinachomsumbua binti yangu ni Usonji”
Tafiti zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kati ya watoto 160, mtoto mmoja anasumbuliwa na tatizo la Usonji. Nchini Rwanda taarifa za watoto wenye tatizo la Usonji ni chache, lakini Bi Rosine Duquesne Kamagaju, Mkurugenzi na Muanzilishi wa Shirika la Usonji nchini Rwanda, alisema kuwa; ‘Kwa sasa idadi ya watoto wenye tatizo la Usonji imeongezeka’
Wazazi ambao wana watoto wenye tatizo la Usonji nchini Rwanda, hawapati fursa kama aliyoipata Bi Jacqueline, hivyo watoto wanakosa masomo. Wazazi hawapati hata nafasi ya kujua kuwa watoto wao wana tatizo la Usonji sababu ya ukosefu wa utambuzi. Bi. Rosine alisema kuwa;
“Watoto wenye Usonji hufukuzwa shule. Familia hupata wakati mgumu kiuchumi, sababu kuongezeka kwa gharama za rasilimali ili kuweza kufundisha watoto wenye tatizo la Usonji”
“Watoto wanaopata elimu sahihi na msaada mapema katika kipindi cha ukuaji wanakuwa na Uwezo, ujuzi na ushiriki mzuri katika mambo ya kijamii. Hawa watoto wanahitaji kujaliwa kwa kupata walimu wenye ujuzi na uzoefu katika utoaji elimu”
Autism Rwanda ni Taasisi pekee nchini Rwanda, inayotoa huduma kwa watoto wenye tatizo la Usonji, lakini hamna mtaala maalumu unaofatwa katika kutoa mafunzo kwa watoto hawa. Bi Joan Murungi, Msimamizi wa Utengenezaji na Uboreshaji wa Mitaala katika Bodi ya Elimu nchini Rwanda alisema kuwa;
“Tumeanza kuandaa mitaala ya watoto wenye ulemavu wa Akili na watoto wenye tatizo la Usonji. Tupo katika hatua ya mwisho ya maandalizi na mwisho wa mwezi tutaanza kutoa machapisho”
“Hatua inayofuata ni kutoa mafunzo kwa walimu lakini tutachagua wachache kutokana na ufinyu wa pesa. Mafunzo ya mtaala mpya yataanza kwa walimu wanaofundisha katika shule maalum ambazo watoto wenye ulemavu wa akili hupelekwa”
Source: https://www.newtimes.co.rw/news/school-curriculum-autistic-children-offing