by Martha Chimilila
Ndoa za Utotoni ni ndoa ambazo hufungwa kabla ya wana ndoa kufika umri wa miaka 18. Ijapokuwa sheria zinapinga ndoa za utotoni, lakini tafiti zinaonyesha ongezeko la vitendo vya uvunjwaji wa sheria vikiendelea ulimwenguni kote. Ndoa za utotoni zinasababisha matatizo makubwa kama Unyanyasaji wa kijinsia, Kupoteza haki ya kupata elimu na matatizo ya Kiafya.
Nchini Rwanda, sera mbalimbali na pesa zilitolewa ili kutekeleza miradi dhidi ya mapigano ya ndoa za utotoni. Tatizo kubwa ni kwamba wanaharakati wa haki za watoto wamekumbana nalo ni kuwa, jamii inayowazunguka watoto hawa ndiyo ina neno la mwisho. Hii inakwamisha utekelezaji wa adhabu kali kwa watu wanaovunja sheria.
Ili kuweza kupata suluhu za kupunguza ndoa za utotoni nchini Rwanda, wadau mbalimbali na wanaharakati wa haki za watoto wanapaswa washirikiane. Maafisa wa serikali wanaweza kuona kuwa hawawezi kutoa mawazo yenye Utatuzi wa tatizo hili ila viongozi wa Jadi wanaweza. Viongozi wa Jadi wanaweza kutoa suluhu ambazo zitaenda na mahitaji yao, suluhu hizi zinaweza pia kutumika kurekebisha shida nyingine zinazosababisha uvunjwaji huu wa haki za Kibinadamu.
Katika nchi nyingi za Kiafrika viongozi wa Jadi wana ushawishi mkubwa kwani wana taarifa muhimu za ushiriki wa wanakijiji na imani zao maana ni watu ambao wanaishi nao. Wao husikilizwa na Kuheshimiwa na wana kijiji, viongozi wa jadi huungwa mkono kwa kile ambacho watakiongea. Kwa hivyo ni muhimu kutoa mafunzo na kuomba msaada wao katika kusaidia kuzuia ndoa za utotoni.
Nini kifanyike ili Kutatua tatizo;
Ni muhimu pia kutoa mafunzo shuleni ili kuongeza uelewa wa mabinti. Wasichana wengi nchini Rwanda hufikiri ni Kawaida kwao kuolewa wakiwa na umri mdogo. Wakipatiwa mafunzo na kufahamishwa athari za kuolewa katika umri mdogo, wataweza kupinga na hata kukata rufaa katika vyombo vya kisheria.
Ushirikishwaji wa viongozi wa dini utasaidia kupunguza tatizo la ndoa za utotoni. Viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika kubadili mitazamo ya waumini wao. Wana uwezo wa kutetea uwezeshwaji na ushiriki wa watoto wa kike katika mijadala ya kijamii, hii itasaidia kubadilisha Mitazamo juu ya maswala ya jinsi na jinsia katika jamii na hii itachangia kuongeza thamani kwa watoto wa kike.
Serikali inapaswa kuanzisha idara vijijini ili kushughulikia ndoa za utotoni. Idara hizi zitasaidia kuanzishwa kwa vilabu vya wasichana ambazo zitasaidia kutoa taarifa na kuongeza uelewa wa athari za ndoa za utotoni. Vilabu hivi vitaweza anzisha miradi mbalimbali ambayo itawasaidia watoto wa kike kupata kipato. Umaskini ni kikwazo kikubwa na ndiyo sababu kuu inayochangia ongezeko la ndoa za utotoni.