By Martha Chimilila
Mfumo wa Haki za Watoto ni kitendo cha wazazi, jamii, serikali na wadau wa maswala ya watoto kusimamia na kulinda maslahi ya watoto kama haki ya kupata elimu bora, lishe yenye tija na afya njema. Kuna mikataba mbalimbali duniani ambayo ilisainiwa kati ya nchi na Mashirika ya Kutetea na Kulinda haki za watoto duniani. Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mfumo wa haki za watoto unasimamiwa na sheria juu ya ulinzi wa watoto (iliyopitishwa mnamo 2009, ilitokana na kampeni ya BICE).
BICE ni Shirika chini ya Kanisa la Katoliki linalofanya kazi ya kusimamia haki za watoto duniani. BICE ilianzisha kampeni ya ‘Utoto bila Magereza’ ambayo ililenga kukuza ulinzi wa watoto wanaokinzana na sheria, kufanya kazi katika shule zao, utaalamu wa kijamii na kurekebisha mahusiano ya kifamilia kwa kukuza na kutetea haki zao za kimsingi. Kampeni ya ‘Utoto bila Magereza’ ilizingatia ukuzaji na uendelezaji wa mifumo ya haki za watoto na kurudisha mazoea yanayolingana na viwango vya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ya haki za watoto.
Kampeni hii ilileta Mapinduzi makubwa na kushinikiza Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kubadili sheria ya kikoloni (1960) ya uhalifu wa watoto, ambayo iliweka umri wa uwajibikaji wa makosa ya jinai kuanzia miaka 16 na adhabu kali dhidi ya watoto, kifungo cha maisha na hukumu ya kifo.
Mabadiliko ya sheria yalisaidia kumuepusha mtoto na kesi ndefu za kimahakama. Sheria ya sasa ina vifungu vya ulinzi wa mahakama, adhabu za kijamii kwa watoto chini ya umri wa miaka 18. Kinshasa, 29 Juni 2011, miaka miwili baada ya kutangaza sheria ya ulinzi wa watoto, takribani watoto 3000 walibaki katika magereza yote nchini Kongo. Maelezo ya Kawaida ya mtoto anayekinzana na sheria huko Kongo ilianzishwa ili kutoa maelezo yafuatayo:
“Kulingana na sheria, ni kinyume cha sheria kuwa na watoto gerezani”
Vincent mtoto wa miaka 16, ambaye yupo chini ya usimamizi wa asasi ya watoto, Ofisi ya Kimataifa ya Watoto Katoliki (BICE) alikuwa gerezani kabla ya kuwasili BICE alisema yafuatayo; “Kila asubuhi ni lazima ufanye kazi, usipofanya hivyo unapigwa, unamwagiwa maji au unafungiwa ndani ya chumba chenye giza. Kama una marafiki au wazazi wanaokujali na kukutembelea basi utapatiwa chakula, la sivyo hautokula kabisa’’
Bwana Innocent Bugandwa, Afisa wa ulinzi wa kisheria wa Mfuko wa Watoto wa UN(UNICEF) alisema yafuatayo kwa IRIN; “Hali ya maisha kwa watoto katika magereza yote nchini (DRC) ni hatari sana. Watoto hawapati huduma za afya, mahusiano na familia hukatwa”
Kufatia utekelezaji wa sheria juu ya Ulinzi wa Watoto, Kulianzishwa mahakama saba maalum kwa watoto wenye umri wa miaka 14 hadi 17. Mnamo tarehe 29 Aprili majaji 12 waliteuliwa kushughulikia sheria ya uhalifu kwa watoto. Hii imesaidia katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kusimamia haki za watoto nchini Kongo.
Source: https://www.refworld.org/topic,50ffbce484,50ffbce4b7,4e1d927a2,0,,,COD.html