Mduara wa Unyanyasaji Nyumbani

Wazazi ndio washawishi wakubwa zaidi katika maisha ya watoto wao.

Kwa hivyo, mienendo ya wazazi huwa na athari kubwa mno kwa watoto wao.

Kwa mfano, Wazazi wanaozushiana na kupigana kila kuchao, hua sumu kwenye maisha ya watoto wao.

swali ni, Sumu hii yaletwa vipi?

Sumu hii huja baada ya wazazi kuwanyanyasa watoto hawa kiakili kwa sababu ya vita visivyoisha, na kurushiana kwa maneno makali kati ya wazazi.

Kuhisi uchungu wa kushuhudia unyanyasaji nyumbani, haina uhakikisho ya kwamba watoto watapitia njia tofauti wakiwa watu wazima, bali kutokana na visa fulani, iwapo watoto watakabiliwa na unyanyasaji wa mapema itawawekea msingi wa kufuata mstari huo huo watakapokuwa watu wazima.

Emily Chebet, mfanyakazi wa kijamii kutoka Uasin Gishu anasema kwamba, athari kwa watoto wakati wa sasa hivi na siku zijazo zaweza kuwa mbaya mno.

Huku akisema kwamba, watoto wengi wanaweza kuwa na masuala ya uaminifu, na hata watashindwa kuridhika na mwenendo wa maisha yao, na wataishi wakizingatia dosari zao, uzembe na kadhalika, na hivyo kuona vigumu kujihusisha na mahusiano ya maana.

Pia wataendelea kuwa na matatizo na familia, marafiki, na wafanyakazi wenza, pia watahisi wamelemewa na matarajio ya wengine juu yao.

“Hii inawafanya wajiskie kana kwamba, wametengwa, hasa na watu walio karibu nao,” aliongeza.

Utafiti wa UN Women mwaka wa 2020 pia uligundua kwamba wavulana wanaofanyiwa unyanyasaji wakiwa wadogo, basi wana uwezekano mkubwa wa kufanya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika siku zijazo.

Ripoti ya Utafiti wa Ukatili Dhidi ya Watoto nchini Kenya (2019) pia iligundua kuwa, wanaume waliokumbana na ukatili iwapo bado ni wachanga, walikuwa na uwezekano mkubwa wa kudhulumiwa katika siku zao zijazo.

“Asilimia 38 ya wanaume walikumbwa na ukatili wa utotoni huku asilimia 29 ya wanawake waliripoti ukatili huo huo,” ripoti hiyo ilisema.

Ripoti ya 2019 ilisema kwamba, wahusika wengi wa vurugu hizi, , walikuwa wazazi, walezi, na jamaa ya karibu.

Uwezekano wa watoto ambao walikabiliwa na unyanyasaji wa kunaswa katika mizunguko ya ukatili uko juu mno, kwani watoto hawa wataendelea kuhalalisha vurugu hizi majumbani mwao, huku wakiona ni jambo lililo sawa kabisa.

Mduara huu huanza wakati bado mtoto yupo mchanga na anakuzwa na mlezi ambae anapenda vurugu, hii huenda ikamfanya mtoto huyo kukua akijua kwamba vurugu ni jambo la kawaida majumbani, na hivyo hatua ya pili ni wakati mtoto huyo atakuwa mtu mzima na kufanya unyanyasaji huo huo kwa watoto wake, na mduara utaendelea kuzunguka hadi utakosa tamati, na hivyo kuendelea kuathiri watoto zaidi na zaidi.

Kulingana na utafiti wa hapo awali wa Shirika la Afya Ulimwenguni, wavulana na wasichana waliobalehe walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuhalalisha unyanyasaji wa kijinsia kuliko wanaume na wanawake wazima, hasa ikiwa watoto hawa walikulia katika nyumba zilizobobea unyanyasaji.

Je ni vipi tutahakikisha kwamba Watoto Wanalindwa Kutokana na Unyanyasaji wa Nyumbani?

Baada ya kujua kwamba vurugu za nyumbani zaweza kuwa na madhara ya kudumu katika mwili, akili na maisha ya baadae ya watoto, ni muhimu pia kujua jinsi tutawakinga watoto ipasavyo dhidi ya unyanyasaji.

Zifuatazo ni njia kadhaa za kumlinda mtoto dhidi ya unyanyasaji wa nyumbani.

La kwanza ni Kuhakikisha kwamba, Usalama unapewa kipaumbele– hii itafanyika aidha kwa waathiriwa kupata usaidizi unaohitajika, na pia kuondoka katika mazingira ya unyanyasaji.

Kwa kufanya hivi, watoto wanaepushwa na unyanyasaji zaidi na pia wanapewa nafasi ya kukua ndani ya miundo yenye afya. 

La pili ni, Kuwafundisha watoto kuhusu maadili na mienendo yenye Afya

Kama tu vile wazazi huongea na watoto wao kuhusu mahusiano ya kimapenzi, basi vivyo hivyo wazazi wanafaa kujizatiti na kuongea na watoto wao kuhusu mienendo ya afya kwenye familia na kushutumu unyanyasaji wa kifamilia na wa aina yeyote ile.

Watoto wanapaswa kufundishwa njia nzuri za kutatua migogoro katika urafiki, jamii na familia kwa ujumla. Ni muhimu kwamba wajifunze njia zinazofaa ambazo wanaweza kuelewana wao kwa wao, huku wakichukua tahadhari kushiriki na kujua ni kwa nini unyanyasaji hauna nafasi katika mahusiano.

La mwisho ni Kumwelimisha mtoto kuhusu Mipaka ya Afya

Njia bora ya kudhibiti uharibifu, na kuzuia mzunguko wa unyanyasaji wa nyumbani ni kwa kuwafundisha watoto mipaka ya afya.

Hii itakuwa hatua katika mwelekeo sahihi. Watoto wanapaswa pia kufundishwa kumwambia mtu mzima anayeaminika kila wakati ikiwa mtu mwingine anawakosesha raha kwenye maisha yao kwa njia yoyote ile.

Mwandishi-Khadija Mbesa

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *