Mbio za Kupunguza Ukatili wa Kijinsia

By Martha Chimilila

Tanzania kama zilivyo nchi nyingi duniani, kuna ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia kwa Watoto, ambao umefichwa na mila, tamaduni na dini. Ijapokuwa wanaharakati wa haki za Watoto nchini Tanzania wamekuwa wakifanya kampeni mbalimbali ili kupinga ndoa za utotoni, tohara na mimba za mapema. Hali ambayo ni tofauti kwa jamii mbalimbali ikiwemo jamii za kifugaji na wale ambao wanaishi mwambao wa pwani kama Pemba, Tanga na baadhi ya jamii za kifugaji.

Kwa wastani, wasichana watatu kati ya watano, huolewa kabla ya kufika miaka 18 na wasichana wanne kati ya watano huacha shule ili waolewe na kujenga familia kama dini na mila zinavyoruhusu. Ndoa za utotoni zinaleta madhara makubwa, kama afya ya akili na ukiukwaji wa haki za binadamu (Watoto), kwani wasichana walioolewa na umri mdogo, wako kwenye hatari kubwa ya kupata fistula na vifo vya kina mama kwani miili yao bado haina uwezo wa kuhimili mzigo wa uzazi.

Aina hizi za ndoa zimeenea zaidi vijijini miongoni mwa kaya maskini. Wazazi huamini kwamba ndoa hizo zinawalinda wasichana dhidi ya ngono na mimba, na kupata usalama wa kifedha kwa kupokea mahari au mifugo, Baadhi ya familia huwatumia wasichana wadogo kama bidhaa. Nyakati zingine jamii humaliza kesi za unyanyasaji wa Watoto kwa kuwaozesha Watoto hao kwa waliwanyanyasa huku wakipewa mifugo au fedha ili kulinda heshima ya familia zao.

Wanaharakati wa haki za Watoto Tanzania wakishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya nchi wanaendesha kampeni mbalimbali kushinikiza vyombo za kisheria kubadili sheria za ndoa “Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 haiwalindi wasichana dhidi ya kuolewa” Sheria hii inaruhusu wasichana wenye miaka 14 kuolewa kwa ruhusa maalum ya wazazi. Katika jamii za kifugaji mifugo ina thamani Zaidi kuliko mtoto wa kike. Nukuu ya msichana wa kimasai aliyeacha shule ili aolewe:

“Matilda H. alipokuwa na miaka 14, baba yake alimwambia kuwa anatakiwa aolewe na mwanaume wa miaka 34 ambaye tayari alikuwa na mke mmoja. Baba yake Matilda alimwambia kwamba amekwisha pokea mahari ya ng’ombe 4 na Shilingi za Kitanzania 700,000, baba yake alimwambia: “Hauwezi kuendelea na elimu yako. Inabidi uolewe kwa sababu huyu mwanaume amekwisha kukulilipia mahari.” Matilda alimbembeleza baba yake amruhusu aendelee na elimu yake, lakini alikataa. Matilda alituambia, “Nina huzuni sana. Sikuweza kwenda shule, mahari ililipwa, na sikuweza kutokumtii baba yangu.” Matilda alisema mama yake alijaribu kutafuta msaada kutoka kwa viongozi wa kijiji ili kuzuia ndoa, lakini “viongozi wa kijiji waliunga mkono uamuzi wa baba yangu kunioza mimi. Sikuwa na cha kufanya. Sikuwa na jinsi ila kukubali kuolewa.” Mume wa Matilda alimfanyia ukatili wa kimwili na kingono”

Mkufunzi mmoja wa maswala ya stadi za Maisha na Ujasiriamali akiwa anawawezesha wakina mama vijana walio na umri kati ya miaka 14 hadi 24 alipata wasaa wa kuongea na mabinti hao ili kupata kujua sababu za kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo. Mmoja wa mabinti hao kwa jina la Asia Mohamed miaka 18 alisema yafuatayo:

  “Niliachishwa shule nikiwa na miaka 12 na kuolewa kwa sasa nina Watoto wanne, mwaka huu nilibeba ujauzito mwingine ingali nina mtoto wa miezi minne na sikua tayari kuzaa maana sina kipato chochote cha kusaidia Watoto wangu na tuzuiwa kutumia uzazi wa mpango tukiaminishwa ni dhambi mbele ya mwenyezi mungu. Basi nikafanya kila njia ili mimba itoke na mimba ilivyotoka nilishukuru mungu sana kwa kitendo hicho

Kitendo hichi kinaonyesha ongezeko la ugonjwa wa akili kwa mabinti wa jamii hii. Hali kama hizi haimpati binti mmoja ila ni kitendo cha Kawaida kuacha shule na kuolewa. Uminywaji wa haki za msingi kama elimu na uhuru wa Kuchagua au kutoa maamuzi kuhusu Maisha yake umefunikwa kwa kivuli cha dini, mila na tamaduni za jamii husika.

Nini kifanyike ili kupunguza tatizo la ukatili wa Kijinsia kwa Watoto?:

Mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu binti wa kuanzia miaka 14 kuolewa, elimu ya athari za mimba za utoto itolewe kwa jamii husika. Elimu ya afya ya uzazi itolewe kwa jinsia zote mbili (wakike na wakiume) pamoja na jamii inayowazunguka wakishirikiana na viongozi wa dini ili kuweza kukemea tatizo hilo hata wakiwa katika maeneo ya kuabudu. Wanaharakati wa haki za Watoto wakishirikiana na wadau mbalimbali wa maswala ya Watoto pamoja na serikali kuunda chombo kitakachosimamia maswala ya ukatili wa kijinsia kwa Watoto itakayo wahusisha na viongozi wa jadi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *