Elimu ni Chachu ya Maendeleo

By Martha Chimilila

Mkoa wa Dar es Salaam, nchini Tanzania kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za msingi wanaorudia madarasa, katika shule za Serikali na zisizo za Kiserikali. Tafiti zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi wanaorudia madarasa imeongezeka mara mbili zaidi katika kipindi cha miaka mitatu. 

Ripoti iliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Msingi (Best) 2020, ilisomwa na Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilionyesha ongezeko la wanafunzi wanaorudia madarasa katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2020. 

Wadau wa Elimu walisema kuwa, kitendo cha kurudia darasa ni moja ya sababu zinazochangia wanafunzi kuacha shule. Kijana Felix Bitambo ni mmoja wa mwanafunzi aliyeacha shule na kuanza kufanya shughuli ndogo ndogo. Hii ilitokea baada ya kurudia darasa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.  

Felix alipoulizwa kwa nini aliacha shule alikuwa na haya ya kusema; 

“Nikiwa darasa la tatu nilirudia, nilipo ingia darasa la nne pia nikarudia na nilipofika darasa la tano walimu walitaka nirudie nikaamua kuacha shule. Kwa sasa nafanya kazi ndogo ndogo maana najua kusoma na kuandika” 

“Kitendo cha kuacha shule kiliwakasirisha wazazi wangu, lakini kwa sasa wananiagiza nifanye shughuli za shambani na kuangalia mifugo. Pia nafanya kazi ya kuendesha pikipiki, natamani kurudi shule kwani nimeelewa umuhimu wa shule” 

Ripoti ya Taasisi ya Elimu ya Msingi (Best)2020, inaonyesha wanafunzi 379,683 walirudia madarasa kwa mwaka 2020 na wanafunzi 189,414 kwa mwaka 2018, idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia 100. 

Wadau wa elimu nchini Tanzania wameeleza kuwa, ongezeko hilo linasababishwa na “uchache na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia”. Ripoti inaonyesha kwa mwaka 2020, wanafunzi wa darasa la tatu na nne ndiyo wanao ongoza kwa kuacha shule. Idadi ya walioacha shule kwa wanafunzi wa darasa la tatu ni 94,687 na kwa darasa la nne ni 117,762 

Bi. Catherine Sekwao, mmoja ya wadau wa elimu nchini, alizungumza na gazeti la Mwananchi akisema;  

“Kitu kinachoweza kupunguza tatizo la kuongezeka kwa wanafunzi wanaoacha shule ni kuongezwa kwa vifaa vya ufundishaji na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi. Vitabu vinapaswa viongezwe mashuleni,maana zamani ilikuwa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu” 

“Umakini na ufundishaji wa walimu unapaswa kuzingatiwa. Zamani hapakuwa na mwanafunzi anayemaliza darasa la kwanza ikiwa hajui kusoma na kuandika. Hii ilitokana na mafunzo maalumu walimu walipatiwa ili kuweza kuenenda na uwezo wa wanafunzi wa darasa la kwanza” 

“Walimu wa siku hizi ni watoro sana, walimu wengi wamekuwa wakipumzika bila sababu ya msingi jambo ambalo linarudisha nyuma uwezo wa uelewa wa wanafunzi kwani wanakosa baadhi ya masomo” 

Bwana Muhanyi Nkoronko, Mtafiti wa Elimu, alisema kuwa;  

“Kila mwanafunzi anaporudia darasa, kwa sisi watafiti tunatafsiri kama ongezeko la gharama kwa Mzazi. Walimu wanapaswa kutoa elimu kikamilifu (ujuzi na maarifa) ili kupunguza gharama za kumpeleka mtoto shule na pia muda wa mtoto kubaki katika ngazi moja ya elimu kwa kipindi kirefu” 

“Serikali iondoe kigezo cha mitihani kama njia ya mwanafunzi kutoka darasa moja kwenda darasa lingine. Serikali inapaswa kuweka vigezo vingine kama kupima maarifa, ijapokuwa kisera tunapendekeza mtoto arudie mara moja na akifeli apandishwe darasa” 

Bwana Gerald Mweli, Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi anayesimamia Elimu alisema kuwa; 

 “Serikali imeimarisha usimamizi wa elimu mashuleni, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanafatiliwa ipasavyo. Hii imeenda sambamba na utoaji wa elimu shirikishi kwa wazazi na walimu, juu ya umuhimu wa kusimamia wanafunzi. Tumeanzisha pia mfumo wa (Early warning dropout system), mfumo huu unamsaidia Mwalimu Mkuu kufahamu mienendo isiyofaa ya wanafunzi” 

Bwana Samweli Moroga, Mkuu wa shule ya Msingi Kinyange, Mkoani Kigoma alisema kuwa; 

“Wanafunzi wanao karirishwa darasani mara nyingi huacha shule na wengine ni aibu ya kurudia darasa. Inawezekana kuwa darasa analorudia yupo mdogo wake. Hali hii inaweza kuisha endapo wazazi watasimamia watoto waende shule kwa kuwasukuma na kuwapa moyo” 

Source: https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/wanafunzi-wanaorudia-darasa-na-athari-za-kuacha-shule-3521460 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *